PRISONS YATUMA UJUMBE HUU KWA GEITA

 KUELEKEA mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Geita Gold ambao utapigwa kesho, Mei 26, Uwanja wa Sokoine,Mbeya, Kocha Mkuu wa Prisons, Patrick Odhiambo amesema wamejipanga vizuri kupata alama tatu.

Prisons imekuwa kwenye mwendo wa kusuasua ndani ya ligi kwenye msimamo ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 24 kibindoni.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa Prisons inapambana kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.

 Odhiambo amesema wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu lakini wachezaji wapo tayari na wanahitaji pointi tatu muhimu.

“Wachezaji wote wapo vizuri hatuna majeruhi, Geita Gold ni timu nzuri inacheza vizuri lakini na sisi tupo imara tunahitaji pointi tatu, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi wasikate tamaa.

“Kupitia mazoezi ambayo tumefanya tuna amini kwamba kila kitu kitakuwa sawa na tutapambana kuweza kupata pointi tatu kwenye mchezo huo ambao tutakuwa nyumbani,”.