MASAU Bwire,Ofisa Habari wa Ruvu Shooting amesema kuwa wameomba kupewa muda wa mapumziko kwa Bodi ya Ligi Tanzania,(TBLP) kwa mchezo wao dhidi ya Azam FC ili waweze kufanya maandalizi kwa kuwa wapo safarini.
Bwire amesema kuwa baada ya kukamilisha mchezo wao juzi kwa sare ya bila ufungana na Kagera Sugar hawakupata muda wa kupumzika zaidi ya kuanza safari kurejea Pwani
“Mchezo wetu dhidi ya Azam FC umepangwa kuchezwa tarehe 24 Uwanja wa Mabatini,sisi tunatoka Bukoba leo, (jana) safari ndefu kweli hivyo tutafika tarehe 23 maana yake ni kwamba hakuna kupumzika sasa katika utaratibu huwa tunaelekezwa tupate masaa 72 ya kupumzika.
“Lakini ukiangalia mechi tumecheza jana, (juzi) saa 3 usiku imeisha saa 4:56 kwa utaratibu hata yale masaa 72 ya kupumzika hayapatikani.
“Tumepeleka maombi yetu Bodi ya Ligi kuweza kuona namna ambacho wanaweza kufanya ili walau tupate muda wa masaa 72 ya kupumzika, kutoka saa 4:56 tulipomalizana na Kagera Sugar mpaka tarehe 24 saa 10:00 jioni mchezo wetu utakapokuwa tutakuwa hatujapumzika.
“Kwa hekima na busara na kwa kudhamini ubora wa ligi na nguvu ya vijana katika kupumzika nina amini kwamba hili litafanyiwa kazi, lakini kwa ujumla tupo safarini tukisema tumeanza mazoezi vijana hawawezi kufanya mazoezi wakiwa ndani ya gari wanasafiri.
“Unaona namna inavyokuwa na ugumu kufikia mafanikio ambayo tunayataka na tunasubiri ili tuone hili litakuaje,” amesema Bwire.
Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda amesema kuwa hawezi kulizingumzia hilo kwa kuwa hayupo ofisini.