TUNAAMINI kwamba kwa muda ambao umeaki kuelekea mechi za hatua ya nusu fainali kila timu inafanya maandalizi mazuri ili kuweza kupata matokeo kwenye mechi ambazo watacheza.
Ni Yanga wao watacheza na Simba na Coastal Union hawa watamenyana na Azam FC katika hatua ya nusu fainali ambayo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Kwa mechi hizi za mwisho wa msimu huwa zinakuwa na matukio mengi ambayo huwa hayapendezi hasa katika suala la matumizi ya nguvu nyingi.
Nguvu ambazo zinatumiwa wakati huu zilipaswa zitumike mwanzo wa msimu sasa kwa kuwa ni muda wa kukamilisha msimu basi ni lazima gia ibadilike.
Mazingira yetu tunayajua na namna ambavyo wachezaji wengi wamekuwa wakisota kwa muda mrefu nje wakitibu majeraha yao.
Hivyo jambo la msingi kwenye mechi hizi muhimu kila mchezaji kuwa makini kwa ajili ya mchezaji mwenzake.
Kila la kheri wachezaji, kila la kheri waamuzi tunaamini sheria 17 zitafuatwa na burudani itatolewa