IMEELEZWA kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco amelazimika kumuongezea kandarasi kiungo wa Zambia, Rally Bwalya kwa ajili ya msimu ujao.
Sababu kubwa inatajwa kuwa ni kutokuwa fiti kwa kiungo mkata umeme Taddeo Lwanga raia wa Uganda.
Kiungo Bwalya alisajiliwa Simba Agosti 15, 2020 akitokea Power Dynamos FC ya kwao Zambia alikuwa anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga.
Habari zimeeleza kuwa pamoja na mkataba wa Bwalya kutarajiwa kuisha katikati ya msimu huu, majeraha ya Lwanga yameufanya uongozi huo kulazimika kumuongeza mkataba ili aweze kusaidiana na kiungo mkabaji atakayekuja kuchukua nafasi yake.
“Kuna wachezaji wengi wanatarajiwa kuachwa mwishoni mwa msimu huu na mmoja wapo ni Lwanga, ambaye hali yake ya afya imeshakuwa ya kutisha tangu alipofanyiwa upasuaji, hivyo uongozi umelazimika kumbakiza Bwalya ndani ya timu ili kulainisha safu hiyo ya kiungo.
“Kocha ameutaka uongozi umpatie mkataba Bwalya kwa sababu bado anaamini kadri anavyopata michezo mingi atakuja kuwa mmoja wa viungo tishio nchini kwani ni kati ya wachezeshaji ambao wanaonekana wa kawaida kama usipoujua ufundi wake,” kilisema chanzo hicho.