KLABU ya Geita Gold leo Mei 22 inatarajiwa kumenyana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ambao wapo nafasi ya pili na pointi zao 50.
Geita Gold chini ya Kocha Mkuu, Felix Minziro imekuwa kwenye mwendo mzuri hasa mzunguko wa pili baada ya kuongeza baadhi ya nyota ikiwa ni pamoja na Juma Nyosso na Kelvin Yondani ambao wameongeza nguvu upande wa ulinzi.
Pia mzawa George Mpole amekuwa na zali la kucheka na nyavu ambapo ni namba moja ndani ya Geita Gold akiwa ametupia mabao 13.
Simba wao mtupiaji wao namba moja ni Meddie Kagere mwenye mabao 7 msimu wa 2021/22.
Minziro amebainisha kwamba anatambua mchezo utakuwa mgumu lakini watapambana kupata pointi tatu.
“Ambacho tunahitaji ni pointi tatu na tunawaheshimu wapinzani wetu kwa namna yoyote ile tutajitahidi kuweza kucheza ili kupata matokeo,”
Tayari mastaa wa Geita Gold wamewasili Uwanja wa CCM Kirumba kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo wa ligi utakaokuwa mubashara Azam TV.