IMEELEZWA kuwa Simba imeanza mazungumzo na mshambuliaji wa Orlando Pirates ya nchini Afrika Kusini, Kwame Peprah raia wa Ghana kwa ajili ya kumsajili kuelekea msimu ujao huku thamani yake ikitajwa kuwa euro 250,000 (Sh mil 608.6).
Simba imepanga kukiboresha kikosi chao ili kifikie malengo ya kufika hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Timu hiyo mara ya pili mfululizo imefika hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa na mara ya mwisho msimu huu ambao walitolewa katika Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates.
Takwimu zake msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini zinaonyesha kuwa amecheza mechi 22 na amefanikiwa kufunga mabao matano pekee, kwa ujumla tangu aanze kucheza ligi hiyo ametumika kwenye michezo 45 na kufunga mabao 14. Huku thamani yake ikiwa ni euro 250,000 hii ni kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarkt.
Kwa mujibu wa mmoja wa mabosi kutoka Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo amesema kuwa Kocha Mkuu Mhispania, Franco Pablo ndiye aliyependekeza usajili wa Peprah ambaye ana umri wa miaka 21 tu na amekuwa akitumia zaidi mguu wa kulia.
Bosi huyo alisema kuwa Pablo amemuona mshambuliaji huyo wakati timu hiyo ilipovaana dhidi ya Pirates katika michezo miwili wa kwanza hapa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na ule wa marudiano waliocheza Afrika Kusini.
Aliongeza kuwa kocha huyo amewasisitiza mabosi wake kuhakikisha wanafakikisha mipango ya kumsajili mshambuliaji huyo kama wanataka kufanya vizuri kimataifa.
“Tayari kocha amependekeza kuachana na washambuliaji wawili wa kigeni ambao ni Kagere (Meddie) na Mugalu (Chris) ambao wameonekana kushuka viwango katika msimu huu.
“Pablo anaamini kuwa kukosa mshambuliaji bora wa viwango vya juu ndiyo sababu ya kutofuzu nusu fainali katika Shirikisho, hivyo ameomba wasajiliwe washambuliaji wawili tishio.
“Hivyo kocha amempendekeza Kwame wa Pirates ambaye huenda wakakutana na kikwazo cha kumpata kutokana na Pirates kuonekana kumuhitaji,” alisema bosi huyo.