BEKI WA KAZI AINGIA ANGA ZA SIMBA

KLABU ya Simba ipo katika mazungumzo na beki la kazi raia wa Cameroon, Jean Jospin Engola kwa ajili ya kuimarisha ukuta wa timu hiyo kuelekea msimu ujao.

Simba huenda ikaachana na mabeki wake wa kati akiwemo Pascal Wawa na Erasto Nyoni, hivyo ipo katika mawindo ya kusajili beki mwingine wa kimataifa kuziba nafasi hiyo.

Akizungumza na Spoti Xtra, wakala wa beki huyo, Moses Grifens Mafulu kutoka katika Kampuni ya Royal Soccer Scout Management, ameweka wazi kwamba, Simba ipo katika mazungumzo na wao kwa ajili ya kuinasa saini ya beki huyo mwenye uzoefu mkubwa Afrika.

“Ni kweli Simba wapo katika mazungumzo na uongozi wetu juu ya kumsajili beki wetu Jeang Engola, kila kitu kwa sasa kipo katika uongozi wa pande zote mbili huku kukiwa bado hakuna muafaka wowote, mazungumzo yanaendelea.

“Nadhani baada ya mwezi mmoja kutoka sasa pengine habari itakuwa ni nyingine katika dili hili kwa kuwa kila kitu kinawezekana haswa kutokana na ukubwa wa Simba na mchezaji mwenyewe kuonesha nia ya kutaka kujiunga na timu hiyo,” alisema kiongozi huyo.

Engola mwenye umri wa miaka 24, amewahi kukipiga katika Klabu ya LA Galaxy inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani kuanzia Machi 2017 hadi Desemba 2018. Yupo vizuri katika kukaba, kupiga pasi na kuanzisha mashambulizi.