SIMBA SC YAMFUATA RASMI LUIS

BAADA ya kuwepo kwa tetesi kwamba Al Ahly ina mpango wa kumtoa kwa mkopo winga wake, Luís Miquissone, inaelezwa kwamba, uongozi wa Simba fasta umemfuata mchezaji huyo kutaka kumrejesha kikosini hapo.

Luis ambaye alikuwa mchezaji wa Simba kwa kipindi cha msimu mmoja na nusu kuanzia Januari 2020 hadi Agosti, 2021, tangu ajiunge na Al Ahly amekuwa hana nafasi kubwa ya kucheza chini ya Kocha Pitso Mosimane.

Winga huyo raia wa Msumbiji, anapata upinzani mkubwa kutoka kwa Percy Tau raia wa Afrika Kusini ambaye ndiye mchezaji anayetegemewa eneo la winga.

Akizungumza na Spoti Xtra moja kwa moja kutoka nchini Mali, meneja wa winga huyo, Djibril Cante, amethibitisha juu ya Simba kuwa katika mazungumzo na uongozi wa Al Ahly kuhitaji kumchukua Luis kwa mkopo.

“Ni kweli uongozi wa Simba unafanya mazungumzo juu ya kumpata Luis Miquissone kwa mkopo ili arejee tena ndani ya kikosi chao, mazungumzo yanafanywa kwa pande zote mbili za uongozi wa timu na uongozi wa mchezaji.

“Hakuna muafaka uliopatikana mpaka sasa, lakini bado mazungumzo yanaendelea, uongozi wa Al Ahly upo tayari kumtoa Luis kwa mkopo kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara,” alisema kiongozi huyo.

Kwa upande wa Simba, Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, alisema: “Masuala ya usajili kwa sasa hatupo tayari kuyazungumzia, tupo kwenye maandalizi ya mechi zilizosalia za ligi na nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Yanga, muda wa usajili ukifika kila kitu kitajulikana.”