MTAMBO WA MABAO POLISI TANZANIA NJE WIKI MBILI

STAA wa Polisi Tanzania, Vitalis Mayanga anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki sita kabla ya kurejea uwanjani kwa sasa akiwa amebakiza wiki mbili.

Mayanga atakuwa nje kwa muda huo akitibu majeraha ambayo aliyapata kwenye mchezo dhidi ya Simba uliochezwa Aprili 10, kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Kwenye mchezo huo wa ligi timu zote ziligawana pointi mojamoja baada ya ubao kusoma Polisi Tanzania 0-0 Simba.

 Msimu huu kwenye ligi kuu Mayanga amefunga mabao sita na ni namba moja kwa utupiaji ndani ya kikosi hicho.

 Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Hassan Juma amesema kuwa Mayanga alifanyiwa upasuaji mdogo wa kidole baada kuvunjika kwenye mchezo wa Simba.

“Baada ya upasuaji mdogo Mayanga alitakiwa kuwa nje kwa wiki sita na hadi sasa amebakiza wiki mbili kurejea uwanjani,” amesema.

Kwenye msimamo, Polisi Tanzania ipo nafasi ya 12 ikiwa imekusanya pointi 27 baada ya kucheza mechi 24.