GEORGE MPOLE NI TOFAUTI NA JINA LAKE KABISA

GEORGE Mpole, mshambuliaji namba moja wa kikosi cha Geita Gold na mzawa namba moja kwa utupiaji Bongo jina lake halisadifu yaliyomo kwenye miguu yake.

Nyota huyo kwa sasa anaongoza chati ya washambuliaji wakali wa kucheka na nyavu huku akiwa anaitwa Mpole kwa jina lakini uwanjani yeye anatupia tu.

Bao pekee la ushindi ambalo alifunga mbele ya Mbeya Kwanza kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Majimaji Songea, Mei 17 limetosha kumfanya awe namba moja na kuipa pointi tatu timu yake.

Nyota huyo amebainisha kwamba bado kazi inaendelea kwa kuwa kitu cha msingi ni ushindi kwa timu sio yeye.

“Ambacho ninakitazama ni ushindi wa timu kwani kila mechi tunahitaji pointi tatu na haziwezi kufikiwa ila kushinda mchezo ambao tunacheza ninaweza kufunga ama kutengeneza nafasi,”.

Anayemfuatia kwa kuwa na idadi ya mabao mengi ndani ya ligi ni Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao 12 na ametoa pasi tatu sawa na Mpole.

Kwenye msimamo Geita Gold imefikisha jumla ya pointi 34 ikiwa nafasi ya 4 baada ya kucheza mechi 24 msimu wa 2021/22.