UBUTU WA VIGOGO BONGO DK 270,SIMBA,YANGA,AZAM

VIGOGO wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa nyakati tofauti wote walipitia kwenye ubutu wa washambuliaji kwenye mechi tatu mfululizo ambazo ni dk 270

Ni mabingwa watetezi Simba chini ya Kocha Mkuu,Pablo Franco waliweza kucheza bila kufunga kwenye mechi tatu mfululizo sasa kisha ikawa kwa Azam FC imefika na sasa ni Yanga.

Rekodi zinaonyesha Simba mechi za Januari 17,2022 ilitunguliwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City kisha Januari 22,2022 walitoshana nguvu na Mtibwa Sugar bila kufungana.

Kaitaba walitulizwa bao 1-0 na Amiss Kiiza wa Kagera Sugar ilikuwa ni Januari 26,2022 hivyo waliyeyusha dakika 270 bila kupata bao lolote mabingwa hao watetezi huku wao wakifungwa mawili na msako wa pointi 9 waliambulia moja.

Ngoma iligeukia upande wa Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Abdi Hamid Moallin ilikuwa ni Februari 22, ubao wa CCM Kirumba ulisoma Biashara United 2-0 Azam FC wakarudi Uwanja wa Azam Complex, Machi Mosi ubao ukasoma Azam FC 0-0 Coastal Union.

Machi 5 walikamilisha mwendo wa dakika 270 bila kufunga baada ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania.

Katika mechi 3, Azam FC ilipoteza mbili na kuambulia sare moja na kwenye msako wa pointi 9 iliambulia pointi moja na safu yake ya ulinzi iliokota mabao matatu kwenye nyavu.

Yanga Aprili 30, ubao ulisoma Yanga 0-0 Simba,Mei 4,2022 Uwanja wa Lake Tanganyika ilikuwa Ruvu Shooting 0-0 Yanga na Mei 9 ilikuwa ni Yanga 0-0 Prisons.

Kwenye msako wa pointi 9, Yanga imeambulia tatu ikiyeyusha pointi 6 mazima na haijafungwa wala kufunga bao kwenye mechi za ligi.