KOCHA NABI APIGA MKWARA KUHUSU UBINGWA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo, kwa kuwaambia waache presha anajua jambo la kufanya ili kuweza kutwaa ubingwa wa ligi.

Kauli hiyo ameitoa mara baada ya wapinzani wao Simba walio nafasi ya pili wakiwa na pointi 49 kupata matumaini ya kutetea ubingwa kufuatia Yanga kupata suluhu tatu mfululizo.

Yanga ilianza kupata suluhu dhidi ya Simba, zikafuatia nyingine mbili dhidi ya Ruvu Shooting na Tanzania Prisons.

 Nabi amesema kuwa ameshajua tatizo lililopo katika timu yake ambalo lilisababisha wapate suluhu kwenye michezo mitatu mfululizo ya ligi.

Nabi amesema kuwa mashabiki waondoe hofu juu ya ubingwa, kwani hautakwenda popote kutokana na mikakati mipya atakayokuja nayo kwa kuanzia mchezo ujao dhidi ya Dodoma Jiji utakaochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

“Kwa sasa mashabiki hawapaswi kuwa na presha zaidi ya kuweza kutulia kwa ajili ya kupata matokeo kwa mechi zetu zijazo.

“Hatujapenda kuwa kwenye mwendo huu ila ni matokeo ambayo yapo kwenye mpira kikubwa ni kuweza kutazama mechi zetu zilizopo,” amesema.