UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa umekuwa na msimu mbaya ndani ya 2021/22 kutokana na kushindwa kupata matokeo wanayohitaji kwenye mechi zake.
Chini ya Kocha Mkuu, Abdi Hamid Moallin juzi ikiwa Uwanja wa Sokoine ubao ulisoma Mbeya City 2-1 Azam FC na kuwafanya wayeyushe pointi tatu mazima.
Msemaji wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa matokeo wanayopata ni mabaya hivyo watajiimarisha zaidi kuwa bora.
“Matokeo ambayo tumeyapata hayajazoeleka,hata wachezaji tulionao hawajazoea kwa pamoja tumekuwa na msimu mbaya,tunazidi kupambana ili kuwa vizuri na tunaendelea kupambana ili tukipata nafasi za kimataifa tuweze kuwa imara zaidi.
“Tangu 2013 tulikuwa hatujawahi kufungwa na Mbeya City hii imekuwa mara ya kwanza kwa Mbeya City kuweza kushinda kwetu kwa kuwa miaka 7 ilikuwa ni mwendo wa sare ama sisi tuwafunge.
“Tulikuwa vizuri eneo la kiungo lakini kwenye eneo la mwisho hatukuwa vizuri kwetu na hili ni eneo ambalo huwa linaamua matokeo kwa kuwa mabeki wa Mbeya City walikuwa imara.
“Goli pekee ambalo tulilipata ilikuwa ni shot on target tuliyopata,pongezi kwa Mbeya City sasa tunarudi Dar kwa ajili ya kurekebisha makosa ambayo tumeyafanya ili kuwa imara zaidi,” alisema.
Azam FC ikiwa imecheza mechi 23 imekusanya pointi 32 ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo.