HAALAND, MAN CITY BADO KIDOGO TU

MTENDAJI Mkuu wa Borussia Dortmund, Sebastian Kehl, amefunguka kuwa dili na hatma ya Erling Haaland itajulikana wiki ijayo.

Haaland amekuwa akihusishwa kujiunga na timu tofauti za Ulaya, ingawa Manchester City ikionekana kuwa katika nafasi nzuri ya kumsajili.

Staa huyo amekuwa kwenye kiwango bora tangu atue Dortmund, Januari 2020 akitokea RB Salzburg ya Austria.

 Mwezi uliopita iliripotiwa kuwa Man City wamefanya makubaliano ya awali na Haaland na fedha ya kumwachia ilikuwa ni kiasi cha pauni 63m. Ingawa inaeleza kuwa kifo cha wakala wake Mino Raiola nacho kilivuruga mambo kwa kiasi fulani.

Kehl alisema suala la staa huyo linatarajiwa kuwekwa wazi wiki ijayo kwani mambo yanaenda vizuri.

“Dili la Erling Haaland? Nafikiri tutalitolea ufafanuzi wiki hii kuhusu Erling kujua nini kinaendelea au mambo yamekuwaje.

“Sababu tunafahamu nini kilichopo ndani ya mkataba wake, mwezi uliopita tulijaribu kuona tunafika mahala fulani na kujua hatma ya Erling mambo haya kwenda vizuri na Mino naye akawa amefariki.”

Hata hivyo, Man City wanatajwa kuwa katika hatua nzuri ya kukamilisha dili la staa huyo na inaelezwa kuwa atakuwa analipwa kiasi cha pauni 500,000 kwa wiki akitua hapo.

Haaland tangu ametua Dortmund amefanikiwa kufunga mabao 85 katika mechi za 88 ambazo amecheza ndani ya klabu hiyo.