UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa utawekeza nguvu kubwa kwenye Kombe la Shirikisho ambalo lipo mikononi mwao na hawatahofia kukutana na wapinzani wao Yanga.
Tayari Yanga imekata tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali inasubiri mshindi wa mchezo kati ya Simba na Pamba ili kujua itacheza na nani hatua ya nusu fainali.
Meneja wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa nguvu ipo ya kutosha kwa timu hiyo kuweza kutetea taji la Kombe la Shirikisho.
“Simba ni timu ambayo ina rekodi ya kufanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho na imetwaa taji hilo mbele ya watani wa jadi na kazi iliyopo kwa sasa ni kuweza kulitetea taji hilo kwa mara nyingine.
“Tunajua kwamba hapa tukishinda mbele ya Pamba tunakwenda kukutana na Yanga hilo tuliliona mwanzo hatuna mashaka nalo tutakwenda nao sawa na tutafanikisha malengo yetu hakuna litakaloshindikana,” amesema Ally.