MCHONGO WA AZIZ KI KUJA BONGO KUKAMILISHWA NA NYOTA HUYU

UNAAMBIWA dili la Stephen Aziz Ki kujiunga na Yanga, lina mkono mkubwa wa nyota wa timu hiyo, Yacouba Songne ambaye ni rafiki yake mkubwa.

Yacouba na Aziz Ki ni marafiki wa muda mrefu ambao wote ni raia wa Burkinafaso ambapo wamewahi kucheza pamoja nchini kwao kabla ya kila mtu kwenda kusaka maisha kwingine.

Chanzo cha ndani kutoka Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, timu hiyo ipo karibu kukamilisha dili la nyota huyo wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, huku Yacouba akiwa na msaada mkubwa wa kusimamia dili hilo kutokana na ukaribu alionao.

“Yanga wamekuwa na mazunguzmo ya muda sasa na Azizi Ki, kwa kiasi kikubwa Yacouba Songne amekuwa akihusika katika usajili huo kutokana na ukaribu wao.

“Yacouba na Aziz ni marafiki na ametumika katika kuwaunganisha viongozi wa Yanga na uongozi wa mchezaji, hivyo bado wapo katika mazungumzo.

“Yanga bado ipo katika harakati za kuhakiksha wanampata Aziz Ki ambaye anamudu vema kucheza kama winga na namba 10, mazungumzo bado yanaendelea kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa,” kilisema chanzo hicho.

Spoti Xtra lilimtafuta Yacouba juu ya Azizi Ki kutua Yanga, alisema: “Aziz Ki ni rafiki yangu na tulicheza wote tukiwa Burkinafaso, kuhusu kuja Yanga, kuzungumzia hilo kwa sasa ni ngumu kwa kuwa bado ni mchezaji wa ASEC, lakini kila kitu kinawezekana.”