IKIWA ni kwa mara nyingine tena mfululizo Tanzania imefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi tisa za Afrika ambazo Kombe halisi la Dunia linatarajiwa kutua nchini Mei 31 mwaka huu, katika ziara rasmi ya kombe inayosimamiwa na kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola ambao ni wadhamini wa mashindano hayo kwa ushirikiano na Shirikisho la soka Duniani (FIFA).
Taarifa rasmi ya uzinduzi wa ziara hiyo umefanyika jana Alhamisi jijini Dar es Salaam ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Coca Cola nchini, Unguu Sulay amesema kwa mara nyingine Tanzania imefanikiwa kupata nafasi ya kulishuhudia kombe hilo kabla halijaenda nchini Qatar katika fainali za mwaka huu
“Sio kila Taifa linapata hii nafasi, Tanzania imekuwa na bahati ya kupata nafasi hii kwa mara ya nne kulipokea kombe hili halisi na watu kupata nafasi ya kupiga nalo picha, kombe hili litakuwa hapa nchini kwa siku mbili kuanzia Mei 31, hadi Juni Mosi likiongozwa na gwiji wa zamani wa Ufaransa, Juventus na Monaco David Trezeguet.
“Huu ni muendelezo wa kampuni yetu sio tu kuishia kuburudisha kupitia vinywaji bora, lakini pia kujihusisha moja kwa moja na msisimko wa kimichezo kupitia soka na burudani.” alisema Unguu.
Naye mgeni rasmi katika uzinduzi huo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa alisema: “Serikali na wizara yetu ya michezo imefarijika na ziara hii ikiwezeshwa na ninyi Coca cola, Rais wetu (Samia Suluhu Hassan), anapenda michezo na tuna ndoto siku moja tuje kuandaa fainali hizi ingawa kwanza tunatakiwa kuamini inawezekana.”
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema: “Coca Cola imekuwa ni mdau mzuri wa kuendeleza soka, sijui kama watu wanafahamu kuwa hata timu yetu ya Taifa Stars ya sasa, ina wachezaji wengi ambao walizalishwa na mkakati wa kuzalisha vijana uliodhaminiwa na kampuni hii na ukaleta matunda bora kwa Taifa letu.”