KILA mafanikio yana zawadi sahihi kutoka kwa Mungu, kauli hii inakamilishwa zaidi na dili nono alilowekewa mezani beki kisiki wa Simba raia wa DR Congo, Henock Inonga Baka na Klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Inonga ambaye alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu, akitokea katika DC Motema Pembe, tayari ameshajitangazia ufalme mkubwa katika nafasi hiyo hasa baada ya kufanikiwa mara mbili kumzuia Fiston Mayele kutetema katika Dabi ya Kariakoo.
Chanzo chetu kutoka Klabu ya Orlando Pirates, kimesema kuwa tayari uongozi wa timu hiyo umeonyesha nia ya kutaka kumsajili Inonga ifikapo mwishoni mwa msimu huu.
“Kwa ofa ambayo nimeiona kwa Orlando Pirates wakiitangaza kwa ajili ya kuifikisha Simba, ili waweze kuinasa saini ya beki wao Inonga, sidhani kama Simba watakuwa na nguvu ya kuitupa pamoja na kwamba hata wao wapo kwenye mtazamo wa kuboresha kikosi msimu ujao.
“Jamaa wameandaa ofa ya dola 300,000 (Sh mil 694.8) ili kupata huduma ya beki huyo raia wa DR Congo jambo ambalo kama watafanikiwa basi ni wazi Simba itamkosa Inonga msimu ujao na hatimaye kulazimika kutafuta mbadala wake pamoja na kiwango chake kizuri cha kumzuia Mayele.”
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ambapo alisema: “Sisi kama klabu ni wazi ikafahamika kuwa, msimu huu hatujafanikiwa kufikia malengo yetu kwenye Ligi Kuu Bara na hata Ligi ya Mabingwa Afrika na Shirikisho.
“Hivyo kinachotakiwa kufahamika ni kuwa, msimu ujao kabla hatujafikiria kuuza mchezaji suala letu la kwanza ni kufanya maboresho makubwa kikosini ili tupate wachezaji watakaotuvusha au kutufikisha kwenye malengo yetu, kwa maana hiyo sidhani kama kuna mtu atakuwa tayari kuachana na mchezaji muhimu kikosini baada ya msimu huu.”