SIMBA WASEMA MAYELE ALIKUWA MZURURAJI UWANJA WA MKAPA

AHMED Ally, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano ndani ya Simba amesema kuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele hakuweza kutamba mbele ya Joash Onyango na Henock Inonga.

Aprili 30,2022 Mayele ambaye ni kinara wa utupiaji ndani ya ligi akiwa na mabao 12 aliweza kubanwa asiweze kutetema kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi uliokamilika kwa sare ya bila kufungana.

Ally amesema kuwa haikuwa kazi rahisi kwa Mayele kuweza kuonekana kwenye mchezo huo kwa kuwa alikutana na watu wa kazi waliokuwa katika majukumu ya kusaka ushindi.

“Ilikuwa ni jambo gumu kwa yule Mayele, (Fiston) kuweza kupenya kwenye ngome yetu, (Simba) kwani alikutana na watu wa kazi ngumu hasa mbele ya Joash Onyango na Henock Inonga ilikuwa kazi kwelikweli.

“Kwa upande wangu sikumuona Mayele uwanjani zaidi mwanzo wa mchezo alionekana akiwaambia mashabiki washangilie ila baada ya hapo nadhani alikuwa anazurula tu uwanjani hata angetoka tungemsindikiza na kumleta mwingine ambaye ni Makambo, (Heritier) ili naye aweze kuzurura,” amesema Ally.

Pia hata washambuliaji wa Simba kwenye mchezo huo ikiwa ni pamoja na Chris Mugalu na John Bocco ambaye aliingia akitokea benchi walishindwa kuifunga Yanga iliyokuwa chini ya Bakari Mwamnyeto.