YANGA:HAO SIMBA NI WAKAWAIDA TU

UONGOZI wa Yanga, umeweka wazi kwamba wapinzani wao Simba ni wa kawaida, hivyo hawana hofu kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa Aprili 30, 2022.

Haji Manara, Ofisa Habari wa Yanga, amesema wachezaji wao wapo tayari na wanatambua kwamba mchezo huo ni muhimu kupata pointi tatu ili kuufikia ubingwa wa ligi hiyo.

“Ipo wazi kwamba (Simba) ni wa kawaida kwa kuwa tumewafunga mara nyingi zaidi na mabao mengi kila ambapo huwa tunakutana nao

“Tumewazidi kwa pointi 13, hilo lipo wazi, tuna mabao mengi zaidi kuliko timu nyingine na tumeweza kuwa na timu ambayo haijafungwa mabao mengi, hivyo tuna kila sababu ya kufanya vizuri.

“Ukitazama tumeshinda mechi nyingi ngumu na zile ambazo hazikuwa na ugumu mkubwa, Coastal Union walikuwa wanatutesa sana pale Uwanja wa Mkwakwani, lakini tumewafunga, Namungo mara tano hatujawafunga, lakini msimu huu tumewafunga.

“Azam FC hawa hatujawahi kuwafunga mara mbili mfululizo, lakini mara hii tumewafunga nje ndani.

“Wapinzani wetu hatuwadharau kwa kuwa wana timu imara ndio maana wameweza kuishia hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, tulipokutana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii tuliwafunga.

“Tunaye mfungaji mwenye mabao mengi ambaye ni Fiston Mayele (12). Malengo yetu ni kuona kwamba tunashinda ubingwa wa ligi na haitawezekana ikiwa hatutashinda mechi ngumu na kupata pointi tatu kwenye kila mechi.

“Kipaumbele chetu kwanza ni kushinda mchezo ujao ili kutwaa ubingwa wa ligi, mashabiki wanahitaji ubingwa na tunahitaji mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi kuujaza uwanja.

“Hii mechi sisi ndio wenyeji, wenzetu sasa hivi wanatia huruma, hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi huu ni mchezo muhimu kwetu.

“Kuna motisha ipo kwa wachezaji na hatuwezi kuitaja kwa sasa kwa kuwa hayo ni mambo ya zamani.”