NAHODHA wa kikosi cha Yanga ambaye ni beki Bakari Mwamnyeto amesema kuwa lengo lao kubwa kwa msimu huu wa 2021/22 ni kuweza kutwaa mataji ili kurejesha furaha kwa mashabiki wa Yanga.
Ndani ya ligi Yanga ambao ni vinara wa ligi walikuwa ni mashuhuda misimu minne mfululizo ubingwa ukielekea kwa watani zao wa jadi ambao ni Simba.
Kwa sasa Yanga imekuwa kwenye mwendo mzuri na inaongoza ligi ikiwa na pointi 54 huku mabingwa watetezi Simba wakiwa nafasi ya pili na pointi zao ni 41.
Mwamnyeto amesema kuwa wanaamini kwamba ushindani uliopo ni mgumu na kila timu inapambana kufanya vizuri hivyo nao wana malengo ya kufanya vizuri.
“Tunajua kwamba ushindani ni mkubwa na kila timu inapambana kufanya vizuri hilo lipo wazi lakini tunahitaji kutwaa ubingwa wa ligi pamoja na makombe kwenye mashindano mengine ambayo tunashiriki,”.
Aprili 30 Uwanja wa Mkapa ,Yanga inatarajiwa kumenyana na Simba kwenye mchezo wa ligi ambao utatoa picha kamili ya nani atakuwa bingwa.
Unakuwa ni mchezo wa mzunguko wa pili baada ya ule wa awali uliochezwa Uwanja wa Mkapa kugawana pointi mojamoja.