SALUM Abubakar Salum, ‘Sure Boy’ kiungo wa kazi ndani ya kikosi cha Yanga ameweka wazi kwamba anaufikiria mchezo wao dhidi ya Simba unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa Aprili 30.
Sure Boy aliweza kuwaka mbele ya waajiri zake wa zamani Azam FC kwenye mchezo wa ligi walipokutana Aprili 6,2022 wakati ubao wa Azam Complex uliposoma Azam FC 1-2 Yanga na aliweza kupiga jumla ya pasi 41.
Mtu wa karibu wa Sure Boy amesema kuwa Sure Boy alikuwa amepanga kucheza kwa umakini mbele ya Azam FC ili asionyeshwe kadi ya njano.
“Sure Boy alisema kwamba hataki kupata kadi ya njano mbele ya Azam FC kwa kuwa alikuwa na kadi mbili na alikuwa anaufikiria mchezo dhidi ya Simba ila bahati mbaya alionyeshwa kadi ya njano.
“NIlimwambia mbona umepata majanga alisikitika sana kwa kudhani kuwa atawakosa Simba ila kwa kuwa hakucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Geita Gold na pia kuna mchezo dhidi ya Namungo basi lengo lake lipo palepale,” alisema.
Haji Manara, Ofisa Habari wa Yanga alisema kuwa hawana hofu na mchezo wao dhidi ya Simba watapambana kupata pointi tatu.
Zimebaki siku 6 kwa watani hawa wa jadi kuweza kukutana Uwanja wa Mkapa kwenye msako wa pointi tatu.