KOCHA Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amethibitisha kiungo mshambuliaji wa klabu hiyo Saido Ntibazonkiza atakosekana kwenye pambano la kesho dhidi ya Namungo kutokana na majeraha.
Akiongea na Waandishi wa Habari kuelekea pambano la kesho Kaze amesema Saido Nitbazonkiza hawezi kuwa sehemu ya kikosi hicho japo viungo wengine waliokuwa majeruhi kama Khalid Aucho na Feisal Salum ‘Fei Toto’ tayari wamerejea.
Viungo hao ambao waliukosa mchezo dhidi ya Azam FC wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kitakachomenyana na Namungo kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Yanga wanakutana na Namungo katika mchezo wa mzunguko wa 20 wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 katika pambano la kwanza lililopigwa katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.