SIMBA:HATUTARUDIA MAKOSA,TUTAFUZU NUSU FAINALI

BAADA ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Orlando Pirates kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba SC wamesema wanakwenda Afrika Kusini kumalizia kazi na wanaamini kwamba hawatarudia makosa.

Jumapili, Aprili 17,Simba iliibuka na ushindi huo katika Uwanja wa Mkapa, Dar, Jumapili ijayo watarudiana nchini Afrika Kusini ambapo mshindi wa jumla atakwenda nusu fainali.

 Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema wana imani hawatarudia makosa ambayo walifanya kwenye hatua hiyo ya robo fainali.

Ally aliongeza kwamba, kilichobaki sasa ni kuona wanakwenda kuzicheza vema dakika tisini za ugenini kumaliza kazi waliyoianza nyumbani.

“Katika mechi za nyuma tulifanya makosa kwenye hatua ya robo fainali lakini kwa sasa tunakwenda kufanya vizuri na kufanyia kazi yale makosa ambayo tumeyafanya.

“Safari hii hatutaki kuwa ngazi kwa ajili ya wengine kuweza kupenya ni sisi wenyewe tutapamana na kusonga mbele kwani nia tunayo na hatua moja imeanza kuonekana.

“Tunaenda kutafuta nafasi ya kufuzu nusu fainali kwani matokeo yoyote ambayo yatahusu ushindi kwetu ni faida,hivyo mashabiki wetu wazidi kutombea”