KUFUATIA kutokuwepo kwenye mipango ya mchezo wa marudiano wa robo fainali dhidi ya Orlando Pirates, benchi la ufundi la Simba limepanga kumuachia programu maalum kiungo mshambuliaji wao Mghana, Bernard Morrison kuhakikisha anakuwa sawa kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga utakaopigwa Aprili 30, mwaka huu.
Simba wanatarajia kuvaana na Orlando Jumapili hii katika mchezo wa mkondo wa pili wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Jumapili iliyopita.
Katika mchezo huo wa Jumapili iliyopita,Aprili 17, Morrison alihusika katika upatikanaji wa bao hilo la Simba baada ya kutengeneza penalti iliyofungwa na Shomari Kapombe.
Morrison anatarajiwa kuachwa kwenye msafara wa Simba utakaoenda Afrika Kusini kutokana na changamoto alizonazo na mamlaka ya uhamiaji ya nchi hiyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Kama ambavyo tulieleza hapo awali kuwa tunatarajia kumkosa Morrison katika mchezo wetu wa kule Afrika Kusini, lakini tunajua tutakuwa na mchezo muhimu dhidi ya Yanga tutakaporejea hivyo benchi la ufundi litaacha programu maalum ya utimamu wa mwili kwa ajili ya mchezo huyo na wote watakaosalia,”.
Kwenye msimamo Yanga ni namba moja ikiwa na pointi 51 huku Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 41.