SIMBA QUEENS YAGOMEA DABI DHIDI YA YANGA PRINCESS

MENEJA wa Simba Queens, Seleman Makanya, amesema kwa sasa hawana tena dabi na Yanga Princess, ni bora wahamie kwa Fountain Gate Princess au JKT Queens.

Makanya amekuja na kauli hiyo akiwa na maana kuwa Yanga Princess wameshakuwa wa kawaida, hiyo ni baada ya Ijumaa kufungwa nyumbani na Fountain Gate Princess mabao 2-3 katika mwendelezo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite (SWPL).

Makanya alianza kwa kuwapongeza Fountain, kisha akatoa ya moyoni kuhusu dabi hiyo: “Hongereni sana Fountain Gate Princess kwa ushindi wa leo dhidi ya Yanga Princess, ilikuwa mechi nzuri na yenye ushindani mkubwa.

“Sasa imefikia mahali tujitafakari kuangalia dabi, sasa rasmi ihamie ama kwa Fountain Gate au JKT Queens, kuanzia leo hatuna tena dabi na Yanga.”

Yanga Princess na Simba Queens zinatarajiwa kukutana Aprili 23, mwaka huu kwenye mchezo wao wa raundi ya pili ya ligi hiyo.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Simba Queens ilishinda 4-1