MZAMBIA AITAKA NAMBA YA YACOUBA YANGA

MSHAMBULIAJI wa Zanaco ya Zambia, Moses Phiri ambaye anahusishwa kujiunga na Yanga amesema kuwa anatamani kuona anavaa jezi namba 10 katika timu mpya atayojiunga nayo kutokana na kuamini kuwa ni namba ya bahati kwake.

Katika klabu ya Yanga jezi namba 10 imekuwa ikivaliwa na Yacouba Songne ambaye alikabidhiwa jezi hiyo tangu alipowasili akitokea Burkina Faso.

Phiri amesema kuwa amekuwa akitamani kuvaa jezi namba 10 kwa kuwa ni jezi ambayo anaamini ni bahati kwake hivyo kama atajiunga na timu yoyote kwa sasa basi ataomba kupewa jezi hiyo.

“Jezi namba 10 kwangu ni kama jezi ya bahati, kabla sijajiunga na Zanaco nilikuwa nikivaa jezi namba kumi lakini mara baada ya kutua hapa nilikuta jezi namba kumi ikiwa na mtu mwingine jambo ambalo ilinibidi nivae namba 9.

“Kwangu sio mbaya jezi namba 9 lakini muhimu kwangu ni kuona naipata tena jezi namba 10 hivyo nitafanya kila liwezekanalo kama nitahamia timu nyingine basi nivae jezi namba 10 kwa kuwa ni jezi ya bahati kwangu naamini hivyo siku zote.

“Kuhusu timu ambayo nitajiunga nayo msimu ujao hilo bado siwezi kuliweka wazi lakini ukweli ni kwamba kuna asilimia kubwa ya mimi kuondoka hapa hivyo kila kitu kitafahamika mwisho wa msimu,” amesema mchezaji huyo.

Yacouba kwa sasa bado hajarejea uwanjani kutokana na kutiu majeraha yake ambayo alipata kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Mkapa ulikuwa ni mchezo wa ligi.