NYOTA wa Klabu ya Azam FC, Shaaban Iddi Chilunda anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki nne baada ya kupata majeraha ya goti wakati timu hiyo ilipokuwa inajiandaa kucheza na Klabu ya DTB mchezo wa kirafiki.
Chilunda aliongozana na Daktari wa Timu Dkt Mwanandi Mwankemwa na kuibukia Cape Town, Afrika ya Kusini kwa ajili ya kufanya vipimo vya MRI kutokana na majeraha hayo.
Baada ya kufanyiwa vipimo hivyo amegundulika kupata madhara ya kuumia Mtulinga (Ligament) wa Kati-Pembeni, hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka Azam FC.
Daktari Robert Nicolas kutoka Hospitali ya Orthopaedic Surgeon Vicente Palloti ambaye anamfanyia uchunguzi amethibitisha kuwa Chilunda hana haja ya kufanyiwa upasuaji lakini anatakiwa akae nje ya Uwanja kwa takribani wiki nne baada ya hapo ataanza kufanya mazoezi mapesi na atakuwa amepona kabisa.
Hakuwa kwenye kikosi cha Azam FC kilichonyooshwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Kwenye msimamo Azam FC ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 28.