SIMBA:WAPINZANI WANA WASIWASI KUPANGWA NASI KIMATAIFA

PABLO Franco, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa wapinzani wao kimataifa katika hatua ya robo fainali ambao ni Orlando Pirates wana wasiwasi kutokana na kupangwa na timu bora.

Jana Aprili 5 nchini Misri ni droo ya mechi za kimataifa ambapo Simba imepangwa kucheza na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Simba iliweza kutinga hatua ya robo fainali kwa kukusanya pointi 10 sawa na RS Berkane iliyokuwa nafasi ya kwanza kwenye kundi D.

Kocha huyo ambaye ni mara ya kwanza kufundisha soka katika bara la Afrika na kuandika rekodi ya kutinga hatua ya robo fainali akiwa kwenye ardhi ya Tanzania amesema:”Ninajua kwamba Orlando ni timu nzuri, kwa kuwa tumepangwa nayo hilo lipo wazi lakini nina amini kwamba hata wao wana wasiwasi kuweza kupangwa na timu bora.

“Jambo ambalo tunafanya ni maandalizi kwa ajili ya mechi hizo na tupo tayari kupata matokeo mazuri kwa kuwa lazima tucheze na lazima tuonyeshe ushindani,”

Pablo anafanya kazi kwa ukaribu na Seleman Matola ambaye ni mzawa katika timu hiyo ambayo kesho ina kazi ya kusaka ushindi mbele ya Coastal Union.