SIMBA NDANI YA TANGA,MKWAKWANI KUKIWASHA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba baada ya kumaliza mchezo wao wa kimataifa dhidi ya USGN kituo kinachofuata ni Aprili 7 dhidi ya Coastal Union.

Kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mkapa Simba ilifanikiwa kuwatoa kimasomaso Watanzania na Afrika Mashariki kiujumla kwa kuweza kutimiza msemo wa ‘Kwa Mkapa Hatoki Mtu’.

Mchezo huu wa Alhamisi ni wa mzunguko wa pili baada ya ule wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa ubao kusoma Simba 0-0 Coastal Union sasa kazi inahamia Uwanja wa Mkwakwani.

Itakumbukwa kwamba beki wa kupanda na kushuka Henock Inonga aliweza kuonyeshwa kadi yake ya kwanza nyekundu akiwa anatumikia Simba baada ya kumpiga na kichwa mchezaji wa Coastal Union.

Tayari leo Aprili 5 msafara wa wachezaji pamoja na viongozi wa Simba umewasili Tanga jiji lenye amani na upendo kuweza kufanya maandalizi ya mwisho.

Ofisa Habari wa Sima, Ahmed Ally amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya kusaka pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo.

Miongoni mwa wachezaji ambao wapo kwenye msafara huo ni pamoja na Aishi Manula, Ally Salim,Kibu Dennis, Pascal Wawa, Sadio Kanoute na Clatous Chama.