ISHU YA MAYELE KUSEPA YANGA YAFAFANULIWA

UONGOZI wa Yanga umefunguka ishu ya mshambuliaji wao wa kati kipenzi cha mashabiki, Fiston Mayele kuhusishwa kujiunga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Yanga wametoa tamko rasmi kuwa mzee huyo wa kutetema hataondoka kutokana na kuwa na mkataba wa kuendelea kukipiga ndani ya klabu hiyo.

Mayele kwa sasa ndiye mshambuliaji tegemeo wa Yanga akiwa ndiye kinara wa upachikaji mabao ndani ya ligi mara baada ya kufunga mabao 10 sawa na Reliants Lusajo wa Namungo.

Kuhusu Mayele kutakiwa na Kaizer Chiefs, Mhamasishaji wa Yanga, Haji Manara, amesema kuwa mchezaji huyo bado ana mkataba wa kuendelea kuitumikia Yanga huku akisisitiza kuwa hakuna timu hapa nchini ambayo itaweza kumsajili mchezaji huyo.

 Dakika 60 Manara alifunguka kila kitu, pamoja na mambo mengine mengi yahusuyo klabu hiyo.

“Mayele ni mchezaji wa Yanga na bado ana mkataba wa kuendelea kuitumikia Yanga na sisi tuwe wakweli tu Yanga mpaka sasa hatujapata ofa kutoka kwa klabu yoyote ambayo inahitaji mchezaji kutoka Yanga.

“Siyo tu kwa Mayele hata kwa wachezaji wengine hatujapata barua hiyo na kuhusu Mayele kusajiliwa na timu nyingine kwa hapa nchini mimi naona wanajidanganya na kama walifanikiwa katika misimu iliyopita kumsajili mchezaji Yanga basi haitawezekana tena.

“Yanga ya sasa hivi hakuna timu kwa hapa nchini wataweza kusajili mchezaji ambaye Yanga inamhitaji hiyo ni kwa kuwa wachezaji wengi wana furaha kucheza hapa na wanapata kila kitu,” alisema kiongozi huyo.

Mkataba wa Mayele unatarajiwa kumalizika Juni, 2023.

Chanzo:Championi