RS BERKANE WAPIGWA FAINI NA CAF KISA SIMBA

KAMATI ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Afrika, CAF imeipiga faini Klabu ya RS Berkane kutokana na vitendo visivyo vya kinidhamu kwenye mechi za Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba.

Taarifa iliyotolewa mapema leo Machi 28 na CAF imeeleza kuwa mechi iliyochezwa Februari 2022, Simba wakiwa ugenini, mashabiki wa RS Berkane waliwashambulia wachezaji wa Simba kwa kurusha chupa.

RS Berkane wamepigwa faini ya dola za kimarekani 8,000 kutokana na kosa hilo lisilo la kinidhamu.

Katika mchezo wa Dar es Salaam, Ofisa wa RS Berkane aliingia uwanjani jambo ambalo lilifanya mchezo kuweza kusimama kwa takribani dakika 5 huku akiwataka wachezaji kuungana naye kugoma kwa madai mwamuzi anawaonea.

Bodi ya nidhamu ya CAF, imeamua kumfungia kwa miezi 12, Majid Madrane kwa kitendo chake hicho cha kuingia uwanjani na kufanya vurugu huku akizuia mchezo.

Kama haitoshi, RS Berkane kama klabu, wamekumbana na faini ya dola 100,000 kutokana na kitendo hicho cha Madrane kuzuia mchezo.

Baada ya mechi hiyo ya Dar es Salaam, RS Berkane waliwasilisha barua ya kulalamika kuonewa jijini Dar es Salaam na malalamiko makubwa yalikuwa kwa mwamuzi Jaques Ndala wa Congo, ambaye anaendelea kutimiza majukumu yake.

Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo uliochezwa Morocco, RS Berkane walishinda kwa mabao 2-0 na nyota wao Tuisila Kisinda aliweza kuyeyusha dk 90 katika mchezo wa pili RS Berkane ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Kisinda aliyeyusha dk 45.