MSHAMBULIAJI wa Yanga, Yacouba Songne anaweza kurejea uwanjani muda wowte kuanzia sasa baada ya kuwa nje kwa muda akitibu goti.
Yacouba aliumia katika mchezo dhidi ya Geita Gold Oktoba 2, mwaka jana ambao Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Jesus Moloko ambapo yeye alitoa pasi ya bao hilo.
Daktari wa Yanga, Youssef Amar, amesema Yacouba kwa sasa yupo sawa na kuanzia Aprili Mosi ataanza mazoezi.
“Yacouba kwa sasa yupo salama na anaendelea vizuri tofauti na hapo awali ambapo hali ilikuwa mbaya zaidi, kwa sasa tunasubiri mpaka Aprili Mosi ndio aanze rasmi mazoezi ya ufiti ambayo ni pamoja na gym.
“Baada ya hapo ataanza mazoezi na wenzake kwa ajili ya kujiandaa kucheza mechi za ushindani ambazo zitakuwa zimesalia msimu huu, tuna imani ataanza kupatikana mapema sana kwa kuwa maendeleo yake ni mazuri,” amesema daktari huyo.