KUELEKEA mchezo wao wa mwisho wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USGN, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco, ameweka wazi kuwa watafanya kila kinachowezekana kushinda mchezo huo, ili kutinga hatua ya robo fainali.
Aprili 3, mwaka huu, Simba iliyo nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi D, wanatarajia kuwa wenyeji wa USGN katika mchezo huo wa sita wa hatua ya makundi unaotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Simba wamefanikiwa kukusanya pointi saba katika michezo yao mitano waliyocheza, wanatakiwa kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya USGN ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali.
Pablo amesema: “Tulitamani kupata matokeo katika mchezo wetu uliopita dhidi ya ASEC Mimosas ili tusiwe kwenye presha kubwa katika mchezo huu wa mwisho dhidi ya USGN, lakini haikuwa hivyo.
“Hayo yamepita na kazi kubwa iliyo mbele yetu kwa sasa ni kuhakikisha tunashinda mchezo ujao na kutinga robo fainali, tunacheza nyumbani mbele ya mashabiki wetu na hatima ya kufuzu kimchezo iko mikononi mwetu, hivyo tutafanya kila linalowezekana kufanikisha hilo kwa kuwa tunaamini hakuna sababu ya kushindwa.”