YANGA KILA KONA WAMEIBANA SIMBA

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wamewabana kotekote mabingwa watetezi wa ligi na Kombe la Shirikisho, Simba kwa kuwa wazi kwamba wanahitaji kushinda kila sehemu.

Kwenye Kombe la Shirikisho, Yanga imetinga hatua ya robo fainali na inatarajiwa kumenyana na Geita Gold na kwenye ligi, Yanga ni namba moja ikiwa na pointi 48 baada ya kucheza mechi 18.

Mabingwa watetezi Simba ni nafasi ya pili wapo kwenye ligi wakiwa na pointi 37 wameachwa kwa jumla ya pointi 11 na kwenye Kombe la Shirikisho wapo hatua ya robo fainali na watacheza na Pamba FC.

 Mkurugenzi wa Mashindano ndani ya Yanga, Thabit Kandoro amesema kuwa wanahitaji ushindi kwenye mashindano yote.

“Kwenye Kombe la Shirikisho tunajua kwamba tutacheza na Geita Gold hilo lipo wazi ni timu nzuri lakini ambacho tunahitaji ni ushindi ili tuweze kusonga hatua inayofuata.

“Huku kwenye ligi pia lengo ni moja kuweza kushinda mechi zetu hilo litatufanya tuweze kutwaa ubingwa hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi tunaamini kwamba kila kitu kitakuwa sawa,” amesema Kandoro.