KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania,Taifa Stars, Kim Poulsen, amesema kuwa Watanzania wanatakiwa kuelewa kuwa wana timu bora sana ya taifa kwa sasa na wanatakiwa kuwa na imani nayo na kutoa sapoti kubwa.
Kim ameyasema hayo baada ya Stars kuibuka na ushindi mbele ya Afrika ya Kati wa mabao 3-1 kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliopo kwenye kalenda ya Fifa uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, ukiwa ni mchezo wa kwanza kati ya mitatu ambayo watacheza.
Kim amesema Tanzania ina timu bora sana ya taifa ambayo inaweza kufanya vizuri kwenye mchezo wowote wa kimataifa na jambo ambalo Watanzania na wapenda soka nchini kote wanatakiwa kutoa sapoti ya kutosha kwenye kila mchezo ambao timu hiyo itacheza kwa sasa
“Nilizungumza kabla ya mchezo kuwa tuna timu bora sana ya taifa, wachezaji bora pengine kuliko nyakati za hivi karibuni, hatukuwahi kuwa nao kwa wakati mmoja.
“Tuna timu ambayo inaweza ikashindana kwenye mchezo wowote wa kimataifa na ikafanya vizuri. Watanzania na wapenda soka wote wanapaswa kuisapoti timu yetu,” amesema Kim.
Stars inajiandaa na michezo ya kufuzu Afcon 2023 ambapo itaanza michezo yake Juni, mwaka huu Kwa Tanzania ni mabao ya Mbwana Samatta, George Mpole na Novatus Dismas waliweza kutupia huku wapinzani wao walipata bao kwa mkwaju wa penalti.