BEKI wa kati wa Simba, Muivory Coast, Pascal Wawa, amewataka mashabiki wa timu hiyo kupunguza presha ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara licha ya Yanga kuongoza ligi kwa pointi nyingi kwa kuwa bado ubingwa upo wazi, hauna mwenyewe.
Wawa ametoa kauli hiyo Yanga ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 48 ikifuatiwa na Simba wenye pointi 37, huku wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya vinara wa ligi hiyo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Wawa alisema kuwa haoni suala la mashabiki wa timu hiyo kuwa na presha ya ubingwa kutokana na kasi ya wapinzani wao, wakati wao wanashiriki michuano ya kimataifa.
“Nadhani suala la kuwa na presha ya ubingwa kwa sasa halipaswi kuwepo kwa mashabiki wetu kwa sababu bado tuna mechi nyingi za kucheza lakini hakuna mwenye uhakika wa kuchukua, isipokuwa wapo ambao wanaongoza ligi tu.
“Kikubwa ni wao kuendelea kutuunga mkono katika mechi zetu za ligi ili tuweze kushinda zote na kuweza kufanikiwa kutetea ubingwa wetu licha ya kuwa na michuano ya kimataifa ambayo tunaendelea kufanya vizuri,” alisema Wawa.