KISA MAYELE SIMBA WAONYWA

KASI ya ufungaji mabao aliyonayo mshambuliaji Mkongomani wa Yanga, Fiston Mayele kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu imemuibua Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mbatha ambaye ameweka wazi kuwa wapinzani wao katika michezo ijayo wakiwemo Simba wajipange kwani Mayele ataendelea kutetema.

Mayele kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC alipiga shuti lililosababisha KMC wakajifunga katika kipigo cha mabao 2-0. Bado ana mabao 10 kwenye ligi akiwa kileleni kwenye chati ya wafungaji, sawa na Reliants Lusajo wa Namungo.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 48 zinazowafanya waendelee kuongoza msimamo wa Ligi Kuu mara baada ya kucheza michezo 18, ambapo ratiba ya michezo yao miwili ijayo ni dhidi ya Azam Aprili 6 na Simba Aprili 30, 2022.

Senzo amesema: “Kwangu sishangazwi na uwezo wa Mayele, huyu ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi tuliowasajili msimu huu, ana nidhamu kubwa na licha ya uwezo anaouonyesha bado anaonyesha jitihada kubwa mazoezini.

“Nadhani wapinzani wetu katika michezo ijayo wanapaswa wajipange, kwani ninaamini Mayele atawafunga sana katika michezo yetu ijayo,”

Chanzo:Championi