KOCHA AZAM FC:TUTAREJESHA BURUDANI MBELE YA NAMUNGO

MACHI 16,2022 leo kikosi cha Namungo FC kitawakaribisha Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Ilulu, Lindi.

Huu ni mchezo wa mzunguko wa pili ambao unatarajiwa kuchezwa majira ya saa 10:00 jioni ukisubiriwa kwa shauku na mashabiki wa timu zote hizo kubwa Bongo.

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Azam FC, Ahamid Moallin amesema kuwa wapo tayari kwa mchezo huo na wanatambua utakuwa na ushindani mkubwa na watarejesha burudani pamoja na ule ubora ambao walikuwa nao awali.

Kwenye mechi tatu za hivi karibuni Azam FC ilikwama kupata ushindi ambapo safu yake ya ushambuliaji haikuweza kufunga bao ndani ya dakika 270.

“Nadhani katika suala la uchezaji, mashabiki wetu wategemee kiwango bora tena kama hapo awali, nadhani ndicho wanachotarajia kutoka kwetu na hilo ndilo jambo ambalo tutawapa hautakuwa mchezo mwepesi kwa kuwa kila timu inahitaji ushindi.

“Ile burudani na ubora ambao ulikuwepo awali nina amini kwamba utaonekana tena kwa kuwa wachezaji wapo tayari,” amesema.

Kwenye msimamo Namungo ipo nafasi ya 3 huku Azam FC ikiwa nafasi ya nne na zote zina pointi 25 baada ya kucheza mechi 17 tofauti ni mabao ya kufunga ambapo Namungo imetupia mabao 21 huku Azam FC ikiwa imetupia mabao 20.