NYOTA wa kikosi cha Yanga Princes, Aisha Khamis Masaka amepata dili la kucheza soka la kulipwa katika Klabu ya BK Hacken FF ya nchini Sweden.
Nyota huyo ni miongoni mwa mastaa ambao walikuwa wakifanya vema kwenye Ligi ya Wanawake Tanzania na alikuwa anaitwa Asha Magoli kutokana na uwezo wake wa kucheka na nyavu.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Yanga imeeleza kuwa hatua hiyo ni kubwa na wamempa hongera Asha kwa kupata timu mpya na kwenda kuanza changamoto mpya.
“Klabu ya Yanga inamtakia kila la kheri mshambuliaji wetu Asha Masaka anakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa bila majaribio kwenye Ligi Kubwa za Wanawake Barani Ulaya.
“Nyoya huyo atakuwa ndani ya Klabu ya BK Hacken FF inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Sweden kwa makubaliano maalumu.
“BK Hacken FF ni Mabingwa wa Ligi Kuu Wanawake Sweden msimu wa 2020 na wamekuwa wakishiriki UEFA Champions League na mwaka huu wametolewa na Manchester City,” ilieleza taarifa iliyotolewa na Yanga.