MENEJA wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amerusha kombora kwa watani zao wa jadi Yanga, baada ya mshambuliaji wao Fiston Mayele kukabidhiwa zawadi yake ya Ng’ombe.
Mayele aliahidiwa zawadi hiyo baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar uliochezwa Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro Februari 23.
Ahmed Ally amerusha kijembe hicho kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kuandika: “Huyo Ng’ombe mngemchinja mkanywa supu na wageni wenu wa Morocco kabla hawajaondoka ingependeza sana”
Kijembe hicho kinahusisha matokeo ya Machi 13, ambapo Simba iliichapa RS Berkane ya Morocco bao 1-0, kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kabla ya RS Berkane hawajawasili nchini baadhi ya wadau wa Yanga walionekana wakijiandaa na ujio wa timu hiyo kutoka nchini Morocco, huku wengine wakionekana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakiwapokea.
Mayele aliahidiwa zawadi wa Ng’ombe na Shabiki wa Yanga, Peter Kanduru anayeishi mkoani Morogoro, baada ya kuifungia timu yake bao la pili dhidi ya Mtibwa Sugar, huku bao la kwanza likipachikwa wavuni na kiungo mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazonkiza.