NABI ANATAKA MABAO YA MAPEMA NDANI YA YANGA

KATIKA kuwavuruga wapinzani wao katika Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi amesema kuwa anahitaji mabao ya ndani ya dakika 10 ili kuweza kujenga hali ya kujiamini.

Hiyo ni moja ya mikakati yake mipya atakayokuja nayo mara baada ya kurejea katika ligi watakapovaana dhidi ya KMC Machi 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Nabi amesema kuwa kikubwa anataka kuona wachezaji wake ndani ya 15 za mwanzo muda wote wawepo katika goli la wapinzani wao mara baada ya mwamuzi wa kati kupuliza kipyenga cha mchezo.

Nabi amesema kuwa lengo la kuwashambulia wapinzani ni kupata bao la mapema huku wakicheza soka safi kwa lengo la kuwapa burudani mashabiki wao wanajitokeza uwanjani kuwasapoti.

Aliongeza kuwa kikubwa kwa washambuliaji wake Fiston Mayele, Said Ntibanzokiza ‘Saido’, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kupunguza papara na badala yake kutuliza akili na kutumia vema kila nafasi watakayoipata uwanjani.

“Tutarejea uwanjani Machi 13, mwaka huu baada ya kupata muda mzuri wa mapumziko, na tutarejea tutakuwa bora na vizuri zaidi ya hapa.

“Hivyo basi nimetoa muda kwa wachezaji wangu kupumzika kwa siku tatu kabla ya kurejea kambini kuendelea na maandalizi mchezo dhidi ya KMC.

“Mara baada ya kurejea kambini nitaendelea kukiboresha kikosi changu kwa kuhakikisha tunarekebisha makosa aliyoyaona katika michezo iliyopita.

“Kikubwa ninataka kuona wachezaji wangu wakicheza bila ya presha yoyote na ili isiwepo hali hiyo ni lazima tupate ushindi wa mapema utakaowaongezea hali ya kujiamini uwanjani,” alisema Nabi.

Yanga imepanga kuendelea kukaa kileleni katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 45 wakifuatiwa na Simba wenye 37 ambao wanapambana kuwaondoa katika nafasi hiyo ya kwanza ili walitetee taji hilo la ubingwa.