MO AFUNGUKIA ISHU YA USAJILI WA ADEBAYO NA MECHI YA KIMATAIFA

RAIS wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji,’Mo’ amesema kuwa wana imani kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya RS Berkane.

Jumapili,  Simba itakuwa na kazi ya kusaka ushindi mbele ya RS Berkane katika mchezo wa Kombe la Shirikisho unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.

Leo Mo alikuwa anazungumza na mashabiki wa Simba pamoja na Watanzania kiujumla kupitia mitandao ya kijamii.

Mo amesema:-“Shabaha yangu ilikuwa katika miaka 10 tuweze kuchukua ubingwa katika mashindano ya kimataifa lakini haijawa hivyo bado tuna nafasi ya kufanya vizuri.

“Kupoteza mbele ya RS Berkane haitupi presha kwa sababu tuliwahi kufungwa na Al Ahly mabao 5 na AS Vita walitufunga mabao 5 lakini tuliweza kutinga hatua ya makundi na kufika robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Mafanikio siyo kitu chepesi kuna hatua na sisi tunataka kuwa bora. Kwa upande wa usajili tutajipanga na watu wetu wa kufuatilia wachezaji wapo tayari kwa ya kukamilisha usajili.

“Adebayo,(Victorean) huyu pia ni mchezaji mzuri nilipigiwa simu na viongozi wa Simba tutazungumza nao hivyo ni jambo ambalo lipo tusubiri na tuone,”.

Mchezo wa kwanza Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane ya Morocco hivyo wanahitaji ushindi kwenye mchezo wao ujao wa kimataifa.