KILE kikombe cha mateso ambacho wachezaji wa Simba walikuwa wanakipitia kwa muda wa dakika 270 bila kufunga kwenye mechi tatu mfululizo sasa kimebebwa jumlajumla na Azam FC.
Ikumbukwe kwamba Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco ilipitia msoto huo Januari 17,2022 iliponyooshwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City kisha kikombe kikaendelea mpaka Januari 22,2022 walipotoshana nguvu na Mtibwa Sugar.
Wakati wakiamini kwamba watarudi wakiwa imara Simba waliibukia Kaitaba na huko walitulizwa bao 1-0 na Amiss Kiiza wa Kagera Sugar ilikuwa ni Januari 26,2022 hivyo walinyooshwa dakika 270 bila kupata bao lolote mabingwa hao watetezi.
Kwa upande wa Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Abdi Hamid Moallin kikombe cha mateso kilianza Februari 22, ubao wa CCM Kirumba ulisoma Biashara United 2-0 Azam FC kisha wakarudi Uwanja wa Azam Complex, Machi Mosi ubao ukasoma Azam FC 0-0 Coastal Union.
Machi 5 walikamilisha mwendo wa dakika 270 bila kufunga baada ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania.
Katika mechi 3, Azam FC imepoteza mbili na kuambulia sare moja na kwenye msako wa pointi 9 imeambulia pointi moja na safu yake ya ulinzi imeokota mabao matatu kwenye nyavu.