MDAMU APEWA ZAWADI YA USHINDI,AZAM YAPOTEZA

WACHEZAJI wa Polisi Tanzania walimpa zawadi ya ushindi mchezaji wao Gerald Mdamu kwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Mdamu yupo nje ya uwanja kwa muda akitibu mguu ambao aliumia baada ya kupata ajali walipokuwa wakitoka mazoezini na timu ya Polisi Tanzania.

Ni bao la Kassim Shaban dakika ya 41 lilitosha kuituliza Azam FC iliyokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex na kuyeyusha pointi tatu mazima.

Mdamu alikuwepo uwanjani kushuhudia mchezo huo na baada ya dakika 90 alipata muda wa kuzungumza na wachezaji wenzake kwa mara nyingine huku wachezaji wakiweka wazi kwamba hiyo ilikuwa ni zawadi kwa Mdamu.

Ikumbukwe kwamba ajali hiyo ilitokea Julai mwaka jana 2021 ilihusisha basi la wachezaji la Polisi Tanzania walipokuwa wakitoka mazoezini.

Ushindi huo unaifanya Polisi Tanzania kufikisha pointi 22 ikiwa nafasi ya 7 huku Azam FC ikibaki na pointi 25 nafasi moja inashuka kutoka ile ya tatu mpaka ya nne.