NYOTA wawili wa Simba ambao ni Chris Mugalu na Kibu Dennis tayari wameanza mazoezi ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu Pablo Franco.
Nyota hao ni mitambo ya kutengeneza mabao kutokana na kuwa na rekodi za kuwa na uwezo wa kutengeneza nafasi za mabao kwenye mechi ambazo wamecheza msimu wa 2021/22.
Mugalu yeye ametengeneza pasi moja na alikuwa nje kwa muda kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
Pia Kibu yeye ametoa pasi mbili za mabao akiwa ametupia mabao matatu kwenye mechi ambazo alicheza kabla ya kuumia na ni chaguo la kwanza la Pablo.
Washambuliaji hao wawili walikosekana katika mechi mbili za kimataifa ugenini ikiwa ni ile ya sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya USGN ya Niger pamoja na ule ambao Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane.
Licha ya kuanza mazoezi kwa washambuliaji hao wawili waliukosa mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United ambao ulichezwa jana Machi 4,2022 Uwanja wa Mkapa.
Sababu kubwa ya nyota hao kuukosa mchezo wa jana dhidi ya Biashara United ni kutokuwa fiti kwa kuwa wamekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutoka na kuuguza majeraha.
Kuelekea kwenye mchezo ujao dhidi ya Dodoma Jiji ni maamuzi ya kocha ikiwa atahitaji kuwatumia.