MAYELE KUPEWA ZAWADI KUBWA AKIWAFUNGA SIMBA

MJUMBE wa Kamati ya Wazee ya Klabu ya Simba, Said Muchacho, amemuahidi kumpatia zawadi ya mbuzi mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele kama atafanikiwa kuifunga Simba katika michezo inayofuata ambayo watakutana.

Ahadi hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya shabiki mmoja wa Yanga kutoka Morogoro kumpa Mayele ng’ombe baada ya kufunga bao dhidi ya Mtibwa Sugar.

Tayari Simba na Yanga msimu huu zimekutana mara mbili, awali ilikuwa katika Ngao ya Jamii, Yanga ilishinda 1-0 kwa bao la Mayele, kisha suluhu ukiwa mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Timu hizo zinaweza kukutana tena katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam endapo zote zitashinda mechi zao za robo fainali, huku pia zikiwa bado hazijacheza mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuchezwa Aprili, mwaka huu.

Ahadi hiyo ya Mzee Muchacho ameitoa pindi alipokutana na Mayele katika mazishi ya Baba wa Mmiliki wa Kampuni ya GSM, Ghalib Said Mohamed, Mzee Said Mohamed yaliyofanyika Machi Mosi, mwaka huu kwenye Makaburi ya Kisutu, Dar.

Akizungumza na Spoti Xtra, mzee Muchacho alisema: “Tayari nimeongea na Mayele, nimemuahidi kumpatia zawadi ya mbuzi kama atafanikiwa kutufunga Simba katika michezo ijayo ya Ligi Kuu na Kombe la FA, ningeweza kumuagizia hata ngamia kutoka nje ya nchi, lakini naamini zawadi ya mbuzi ni nzuri kwake.”