LEO ni leo kwa Azam FC kusaka pointi tatu muhimu mbele ya Polisi Tanzania ambayo nayo inapiga hesabu ya kusepa na pointi hizo tatu.
Ikumbukwe kwamba jana Polisi Tanzania wachezaji wote pamoja na viongozi wa timu hiyo waliweza kumtembelea mchezaji wao Gerald Mdamu ambaye alipata ajali na aliweza kuwapa ujumbe wa kuwaomba wachezaji wenzake wazidi kupambana.
Huu ni mzunguko wa pili na timu hizo zinatarajiwa kuwa kwenye kazi ya kusaka pointi tatu kwenye mchezo huo unaoatarajiwa kuchezwa saa 1:00 usiku.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa kwa mechi ambazo wanacheza Uwanja wa Azam Complex huwa inakuwa ngumu kupoteza lakini wanawaheshimu wapinzani wao.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu kwa sababu ni timu imara lakini kwa mechi ambazo tunacheza Uwanja wa Azam Complex tumekuwa tukipata matokeo chanya,” amesema.
Hassan Juma, Ofisa Habari wa Polisi Tanzania amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo na wanachohitaji ni pointi tatu.
“Tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo dhidi ya Azam FC tunatambua kwamba utakuwa mchezo lakini tupo tayari kwa ajili ya kuweza kupata pointi tatu,” amesema.