>

MASAA 48 YATENGWA NA KOCHA SIMBA KUSUKA KIKOSI

PABLO Franco Kocha Mkuu wa Simba ametenga siku mbili sawa na saa 48 za vijana wake kupata ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United ambao unatarajiwa kuchezwa leo Uwanja wa Mkapa.

Ikumbukwe kwamba Machi Mosi 2022 kikosi cha Simba kiliweza kurejea nchini baada ya kuwa Morocco kwenye mechi ya kimataifa na walimenyana na RS Berkane katika mchezo wa tatu wa Kombe la Shirikisho Afrika ambao ulimalizika kwa kufungwa mabao 2-0.

Timu hiyo mara baada ya kurejea nchini, moja kwa moja kikosi hicho kiliingia kambini tayari kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United utakaopigwa leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema Kocha Pablo amepanga kuzitumia vema siku mbili ambazo ni Jumatano na Alhamisi kwa ajili ya kukiandaa kikosi chake ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Ally alisema mchezo huo ni muhimu kwao kupata ushindi yatakayorejesha hali ya kujiamini na morali wakielekea katika michezo yao ya Shirikisho dhidi ya Berkane, US Gendarmarie watakayocheza Uwanja wa Mkapa, sambamba na wa ugenini dhidi ya ASEC Mimosas.

“Tumetoka kupoteza ugenini dhidi ya Berkane, hii michuano mikubwa Afrika ndivyo inavyokuwa, kila timu inashinda nyumbani kwake, zamu yetu inakuja na sisi tutashinda nyumbani kwetu.

“Kiukweli safari ilikuwa ndefu, tunashukuru tumerejea salama nchini, wachezaji wamechoka watapata muda wa kupumzika tayari kujiandaa dhidi ya Biashara.

“Kocha amepanga kutumia siku mbili Jumatano na Alhamisi kwa ajili ya kukiandaa kiosi chake vema huku akiwapa muda mzuri wa kupumzika kwa ajili ya kutoa uchovu walioupata tayari kwa ajili ya michezo ijayo ya ligi ukiwemo huu unaofuatia dhidi ya Biashara,” amesema Ally.

Siku hizo mbili tayari zimekamilika hivyo leo ni siku ya kuonyesha kazi kwa vitendo kwenye mchezo huo unaoatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Karume Mara, ubao ulisoma Biashara United 0-0 Simba na kuwafanya wagawane pointi mojamoja.