KAMA utakuwa unaitafuta Yanga ilipo kwa sasa kwenye msimamo ni namba moja na pointi zake kibindoni ni 42 baada ya juzi kushinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Mkapa.
Ilikuwa ni msako wa pointi tatu kwa timu zote mwisho Yanga wakasepa na pointi tatu mazima na ilikuwa namna hii :-
Makipa kazini
Kipa wa Yanga, Diarra Djigui alianza kazi mapema kipindi cha kwanza kwa kuweza kuokoa hatari 8 na kuliweka lango salama na Ramadhan Chalamanda aliweza kuokoa hatari sita langoni mwake katika hizo ni ile moja iliyopigwa na Fiston Mayele dakika ya 26.
Kipindi cha pili Diara aliweza kuokoa hatari tatu langoni mwake huku Chalamanda akiweza kuokoa hatari 7 ilikuwa ni pamoja na mbili za Mayele dakika ya 56 na 80 na moja ilikuwa ya Said Ntibanzokiza dakika ya 82.
Licha ya kuweza kuokoa hatari 13 bado hakuwa na chaguo kwa kuwa alitunguliwa mabao matatu kwenye nyavu zake na kuziacha pointi tatu Uwanja wa Mkapa.
Mapigo huru miguuni mwao
Ni Ntibanzokiza kwa Yanga alipewa jukumu la kupiga mipra iliyokufa kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Said alipiga faulo 3 dk ya 12,38 na 50, kona 2 dk ya 24 na 47 na katika hizo ile ya dk ya 12 ililelnga lango.
David Luhende alikuwa na jukumu hilo alifanya hivyo dakika ya 4 na 34 alipiga kona dk 11 pia Dickson Mhilu naye pia alipiga faulo moja dk ya 7.
Walikosa mabao ya wazi
Djuma Shaban nyota wa Yanga alikosa nafasi 3 za kumtungua Chalamanda kwenye mchezo wa juzi ilikuwa ni dk ya 15,16 na dk ya 24.
Ni Hassan Mwaterema alifanya jaribio kali dk ya 7 halikuweza kuzama nyavuni na Meshack Abraham alikosa nafasi ya kufunga dk ya 41.
Wazee wa kucheza faulo
Dickson Ambundo alikuwa kwenye mchezo wa juzi na aliweza kucheza faulo 2 ilikuwa dk ya 2 na 36 kwa Kagera Sugar miongoni mwa waliocheza faulo ni pamoja na Yusuf Lwanga ambaye alifanya hivyo dk ya 50.
Kiiza mambo magumu
Amis Kiiza nyota wa Kagera Sugar mambo yalikuwa magumu kwake kwenye mchezo huo na alitumia dk 55 Uwanja wa Mkapa.
Kutokana na ugumu wa mchezo hakuweza kufanya jaribio ambalo lilikwenda lango la Diarra ndani ya dk hizo alizotumia.
Waliamua mchezo
Said Ntibanzokiza ambaye alifunga bao moja na Fiston Mayele aliyetupia mabao mawili kwa Yanga hawa waliamua matokeo yawe kwa namna gani Uwanja wa Mkapa.
Mayele anafikisha jumla ya mabao 9 kwenye upande wa kutupia na ni namba moja kwa watupiaji wa Yanga.
Maneno ya makocha
Francis Baraza, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar alisema kuwa walikosea kwenye mchezo huo jambo lililofanya wakaadhibiwa.
“Tulikosea kwenye mchezo wetu tukaadhibiwa,ilikuwa tunahitaji kucheza kwa kukimbizana hilo lilituponza na tulipofungwa bao moja ikatuvuruga kabisa, lakini tutarudi kwenye ubora,” .
Nasreddine Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga alisema kuwa alikutana na timu iliyokuwa na mabadiliko makubwa.
“Ilikuwa ni timu tofauti na ile ambayo tulikutana nayo mzunguko wa kwanza, pongezi kwa wachezaji na ushindi umepatikana lakini haikuwa rahisi,” alisema.